DINI SAFI ILIYOSHIKA MYOYO SEKOU-TOURE, MWANZA.
WANAWAKE wa Idara ya Dorkas ya Kanisa la Kirumba, jijini Mwanza, wamewashauri wagonjwa wa Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure, wasiache kumwomba Mungu wanapokumbwa na maradhi ili awafariji na kurejesha afya zao katika hali njema.
Mkuu wa Dorkas, Mary Joshua, alisema wakati wanawake hao walipozulu wagonjwa hospitalini hapo kwamba, siyo Mungu aletaye maradhi kwa watu,bali ni Shetani asababishaye afya mbaya kwa watu.
WANAWAKE hao Dorkas walifika hospitalini hapo kuwafadhili wagonjwa kwa kuwapelekea chakula,maji ya kunywa, maji ya matunda(juice),matunda yenyewe,mafuta ya kupaka, sabuni na vitabu ambavyo vilikuwa na thamani ya shilingi 540,000.
Vitabu vilivyopelekwa kwa wagonjwa hao ni SABATO YA KWELI, lengo likiwa ni kuwafikishia wagonjwa hao ujumbe wa Sabato.
Miongoni mwa wagonjwa waliofikiwa, alikuwepo mtoto aliyenusurika kufa kwa moto,baada ya nyumba yao kuteketezwa kwa moto ambao ulisababisha wazazi wao kufariki dunia katika ajali hiyo.
Mtoto huyo ambaye amelazwa katika Hospitali hiyo,alijitoa mhanga kuwaopoa wadogo zake, hali iliyomsababishia kuungua mwili mzima.
Muuguzi wa zamu katika Hospitali hiyo, Lucy Washa, ameyaomba Mashirika mengine, zikiwemo Taasisi za kidini kuwaiga akina mama hawa wa Dorkas,Kirumba kuiga kitendo chao cha kuwatembelea wagonjwa na kuwasaidia kama walivyofanya hawa Dorkas.
“Na mashirika mengine ya kiraia,yakiwemo mashirika ya dini, wakiwaiga hawa Dorkas kuja kuwasaidia wagonjwa hospitalini,watapunguza maumivu yao,watawafariji na kupunguza mahitaji waliyonayo”,Lucy Washa alisema.
Katibu wa Dorkas,Kirumba, Felister Chamfora, amesema Dorkas hawataishia hapo,isipokuwa wana mipango kamambe ya kutembelea sehemu mbalimbali ili kuwaona wahitaji kuwafariji na kuwafadhili pamoja na kuwaambia HABARI NJEMA ya Marejeo ya Kristo.